SWISSAID Publications SWISSAID - SWTA 6 - Kitini cha kilimo hai Benki_za mbegu za jamii
Published: 20.11.2019
Benki za mbegu za jamii ni taasisi zisizo rasmi, zinazoongozwa na kusimamiwa na wakulima au serikali za mitaa na vijiji ambayo kazi ya msingi ni kuhifadhi mbegu kwa ajili ya matumizi ya ndani.
Benki hizi zinapatikana katika maeneo mengi duniani na zimekuwepo kwa miaka mingi zikiwa na lengo la kuhifadhi, kurejesha, kuimarisha, na kuboresha mifumo ya mbegu ya ndani.
Hapa nchini mwamko wa wanajamii kuanzisha na kusimamia benki za mbegu ni mdogo. Benki hizi zilikuwa zinapatikana katika maeneo machache ya Dodoma na Mbeya. Benki hizi zinajulikana kwa majina mbalimbali: benki za mbegu/jeni za jamii, nyumba za mbegu za wakulima, vibanda vya mbegu, vikundi vya kutunza mbegu, ushirika au mtandao wa kutunza mbegu, hifadhi ya mbegu za jamii, maktaba ya mbegu, na benki ya mbegu za jamii.
Wakulima wanaoendesha benki za mbegu za jamii huhifadhi mbegu za mazao ya aina mbalimbali zikiwemo zile zinazolimwa kwa wingi mfano mahindi, mpunga n.k. Pia wanahifadhi mbegu za mazao yanayolimwa kwa uchache kama vile mtama na mazao ambayo walaji wameyatelekeza kama vile viazi vikuu. Mbegu hizi zinaweza kuhifadhiwa kwa kiasi kidogo au kikubwa kulingana na hitajio na upatikanaji wake.