Điều này Publication Issue không tồn tại trong ngôn ngữ của bạn, Xem trong: Kiswahili (sw),
Hoặc dùng Google Translate:  

Mbegu ni sehem ya mmea ambayo hutumika kuzalisha/kuotesha mmea mwingine, yaweza kuwa ni zao la ua au sehem ya mmea iliyokomaa na kuwa tayari kuendelea kuoteshwa tena, mfano vipando vya muhogo Mbegu ni mojawapo ya pembejeo muhimu katika kilimo. Mbegu za daraja la kuazimiwa ubora (QDS) ni mojawapo wa vyanzo bora vya mbegu vya kutegemewa na wakulima. Mfumo wa uzalishaji wa mbegu bora za kuazimiwa ubora ulianzishwa na shirika la kilimo na chakula duniani (FAO) mwaka 1993 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2006.

Mbegu hizi ziliingizwa kwenye mfumo rasmi wa kuzalisha mbegu katika sheria ya mbegu ya mwaka 2003, pamoja na kanuni, miongozo na taratibu zake za uzalishaji za mwaka 2007. Mbegu hizi huzalishwa na mkulima mmoja mmoja au kikundi cha wakulima kilichosajiliwa na kupata mafunzo kwa ajili ya kuzalisha mbegu kwa matumizi yao binafsi na/au kuuza kwa wakulima wa maeneo ya jirani. Ni muhimu nasaba/asili ya mbegu hiyo ijulikane na hivyo mbegu ya msingi au iliyothibitishwa kuwa ndizo pekee zinazotumika katika uzalishaji ili kuhakikisha ubora wa mbegu.

Hapa nchini mbegu zilizopevushwa kiasili (OPV) ambazo zinapatikana katika orodha ya taifa ya mimea ndizo zinazoweza kutumika katika uzalishaji wa mbegu za daraja la kuazimiwa ubora na siyo mbegu za kizazi cha kwanza cha mbegu chotara (F1 Hybrids). Mfumo wa mbegu za daraja la kuazimiwa ubora huwawezesha wakulima kupata mbegu bora kwa gharama nafuu na kwa wakati. Mfumo huu wa QDS upo si kwa nia ya kuubadili mfumo rasmi wa uzalishaji mbegu zilizothibitishwa ubora ila kujaza pengo lililoachwa na mfumo rasmi. Ni mfumo unaowahusu wakulima wadogo wadogo walio kwenye vikundi kwa matumizi yao ndani ya wilaya husika.